1 Hili ndilo neno la BWANA lililomjia Hosea, mwana wa Beeri, siku za Uzia, na Yothamu, na Ahazi, na Hezekia, wafalme wa Yuda; na siku za Yeroboamu, mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli.
2 Hapo kwanza BWANA aliponena kwa kinywa cha Hosea, BWANA alimwambia Hosea, Enenda ukatwae mke wa uzinzi, na watoto wa uzinzi; kwa maana nchi hii inafanya uzinzi mwingi, kwa kumwacha BWANA.
3 Basi akaenda akamwoa Gomeri, binti Diblaimu; naye akachukua mimba, akamzalia mtoto mwanamume.
4 BWANA akamwambia, Mwite jina lake Yezreeli; kwa maana bado kitambo kidogo, nitaipatiliza nyumba ya Yehu damu ya Yezreeli, na kuukomesha ufalme wa nyumba ya Israeli.
5 Tena itakuwa siku ile, nitauvunja upinde wa Israeli katika bonde la Yezreeli.
6 Akachukua mimba tena, akazaa mtoto mwanamke. BWANA akamwambia, Mwite jina lake Lo-ruhama; kwa maana sitairehemu nyumba ya Israeli tena, nisije nikawasamehe kwa njia yo yote.