1 Israeli alipokuwa mtoto, nalikuwa nikimpenda, nikamwita mwanangu atoke Misri.
2 Kadiri walivyowaita ndivyo walivyoondoka na kuwaacha; waliwatolea dhabihu Mabaali, na kuzifukizia uvumba sanamu za kuchonga.
3 Lakini nalimfundisha Efraimu kwenda kwa miguu; naliwachukua mikononi mwangu; hawakujua ya kuwa naliwaponya.
4 Naliwavuta kwa kamba za kibinadamu, kwa mafungo ya upendo; nami nalikuwa kwao kama hao waondoao kongwa tayani mwao, nikaandika chakula mbele yao.
5 Hatarudi tena nchi ya Misri; bali huyo Mwashuri atakuwa mfalme wake; kwa sababu walikataa kurejea.
6 Na upanga utaiangukia miji yake, utayaharibu makomeo yake na kuyala, kwa sababu ya mashauri yao wenyewe.
7 Na watu wangu wamejipinda kuniacha; ingawa wawaita kwenda kwake Aliye juu, hapana hata mmoja atakayemtukuza.