1 Njoni, tumrudie BWANA; maana yeye amerarua, na yeye atatuponya; yeye amepiga, na yeye atatufunga jeraha zetu.
2 Baada ya siku mbili atatufufua; siku ya tatu atatuinua, nasi tutaishi mbele zake.
3 Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua BWANA; kutokea kwake ni yakini kama asubuhi; naye atatujilia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyweshayo nchi.
4 Ee Efraimu, nikutendee nini? Ee Yuda, nikutendee nini? Kwa maana fadhili zenu ni kama wingu la asubuhi na kama umande utowekao mapema.
5 Kwa sababu hiyo nimewakata-kata kwa vinywa vya manabii; nimewaua kwa maneno ya kinywa changu; na hukumu yangu itatokea kama mwanga.