1 Ufunuo wa neno la BWANA kwa Israeli kwa mkono wa Malaki
2 Nimewapenda ninyi, asema BWANA. Lakini ninyi mwasema, Umetupendaje? Je! Esau siye ndugu yake Yakobo? Asema BWANA; ila nimempenda Yakobo;
3 bali Esau nimemchukia na kuifanya milima yake kuwa ukiwa, na urithi wake nimewapa mbweha wa nyikani.
4 Ijapokuwa Edomu asema, Tumepondwa-pondwa, lakini tutarudi na kupajenga mahali palipoachwa hali ya ukiwa; BWANA wa majeshi asema hivi, Wao watajenga, bali mimi nitaangusha; na watu watawaita, Mpaka wa uovu, na, Watu ambao BWANA anawaghadhabikia milele.
5 Na macho yenu ninyi yataona, nanyi mtasema, BWANA ndiye mkuu kupita mpaka wa Israeli.
6 Mwana humheshimu baba yake, na mtumishi humcha bwana wake; basi, kama mimi ni baba yenu, heshima yangu iko wapi? Na kama mimi ni bwana wenu, kicho changu ki wapi? BWANA wa majeshi awauliza ninyi, enyi makuhani, mnaolidharau jina langu. Nanyi mwasema, Tumelidharau jina lako kwa jinsi gani?