4 Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zitakapopendeza mbele za BWANA, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani.
5 Nami nitawakaribieni ili kuhukumu; nami nitakuwa shahidi mwepesi juu ya wachawi, na juu ya wazinzi, na juu yao waapao kwa uongo; na juu yao wamwoneao mwenye kuajiriwa, kwa ajili ya mshahara wake, wamwoneao mjane na yatima, na kumpotosha mgeni asipate haki yake, wala hawaniogopi mimi, asema BWANA wa majeshi.
6 Kwa kuwa mimi, BWANA, sina kigeugeu; ndio maana ninyi hamkuangamizwa, enyi wana wa Yakobo.
7 Tokea siku za baba zenu mmegeuka upande, mkayaacha maagizo yangu, wala hamkuyashika. Nirudieni mimi, nami nitawarudia ninyi, asema BWANA wa majeshi. Lakini ninyi mwasema, Turudi kwa namna gani?
8 Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu.
9 Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote.
10 Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.