6 Kabla haijakatika kamba ya fedha;Au kuvunjwa bakuli la dhahabu;Au mtungi kuvunjika kisimani;Au gurudumu kuvunjika birikani;
7 Nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa,Nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa.
8 Mhubiri asema, Ubatili mtupu; mambo yote ni ubatili!
9 Walakini, kwa sababu huyo Mhubiri alikuwa na hekima, aliendelea kuwafundisha watu maarifa, naam, akatafakari, akatafuta-tafuta, akatunga mithali nyingi.
10 Huyo Mhubiri akatafuta-tafuta ili apate kuona maneno yapendezayo, na yale yaliyoandikwa kwa unyofu, yaani, maneno ya kweli.
11 Maneno yao wenye hekima huwa mfano wa michokoo; na kama misumari iliyogongomewa sana; ndivyo yalivyo maneno yao walio wakuu wa makusanyiko, ambayo yatoka kwa mchungaji mmoja.
12 Tena, zaidi ya hayo, mwanangu, kubali maonyo; hakuna mwisho wo wote wa kutunga vitabu vingi; na kusoma sana huuchosha mwili.