1 Lakini ikawa, Sanbalati aliposikia ya kwamba tulikuwa tukiujenga ukuta, akaghadhibika, akaingiwa na uchungu sana, akawadhihaki Wayahudi.
2 Akanena mbele ya nduguze na mbele ya jeshi la Samaria, akisema, Wayahudi hawa wanyonge wanafanyaje? Je! Watajifanyizia boma? Watatoa dhabihu? Au watamaliza katika siku moja? Je! Watayafufua mawe katika chungu hizi za kifusi, nayo yameteketezwa kwa moto?
3 Basi Tobia, Mwamoni, alikuwa karibu naye, akasema, Hata hiki wanachokijenga, angepanda mbweha, angeubomoa ukuta wao wa mawe.
4 Sikia, Ee Mungu wetu; maana tunadharauliwa; ukawarudishie mashutumu yao juu ya vichwa vyao, ukawatoe watekwe katika nchi ya uhamisho;
5 wala usiusitiri uovu wao, wala isifutwe dhambi yao, mbele zako; kwa maana wamekukasirisha mbele ya hao wanaojenga.
6 Basi tukaujenga ukuta; nao ukuta wote ukaungamanishwa kiasi cha nusu ya kimo chake; maana watu walikuwa na moyo wa kufanya kazi.
7 Lakini ikawa, Sanbalati, na Tobia, na Waarabu, na Waamoni, na Waashdodi, waliposikia ya kuwa kazi ya kuzitengeneza kuta za Yerusalemu inaendelea, na ya kuwa mahali palipobomoka panaanza kuzibwa, basi wakaghadhibika mno;