9 Lakini nyinyi ni ukoo mteule, makuhani wa Mfalme, taifa takatifu; watu wake Mungu mwenyewe, mlioteuliwa kutangaza matendo makuu ya Mungu aliyewaiteni kutoka gizani, akawaingizeni katika mwanga wake mkuu.
10 Wakati mmoja nyinyi hamkuwa watu wa Mungu, lakini sasa nyinyi ni watu wake; wakati mmoja hamkupewa huruma ya Mungu, lakini sasa mmepokea huruma.
11 Wapenzi wangu, nawasihi nyinyi kama wageni na wakimbizi hapa duniani! Achaneni na tamaa za mwili ambazo hupingana na roho.
12 Mwenendo wenu kati ya watu wasiomjua Mungu unapaswa kuwa mwema kabisa, ili hata watakapowasingizieni kwamba mnatenda mabaya, waweze kutambua matendo yenu mema na hivyo wamtukuze Mungu siku ya kuja kwake.
13 Basi, jiwekeni chini ya mamlaka yote ya kibinadamu, kwa ajili ya Bwana: Utii kwa mfalme aliye mtawala mkuu,
14 utii kwa wakuu wa mikoa ambao wameteuliwa naye kuwaadhibu wahalifu na kuwasifu watendao mema.
15 Maana Mungu anataka muweze kuyakomesha maneno ya kijinga ya watu wasio na akili kwa matendo mema mnayofanya.