13 Mbele ya Mungu anayevipa vitu vyote uhai, na mbele ya Yesu Kristo aliyetoa ushahidi na kukiri ukweli mbele ya Pontio Pilato,
14 nakuamuru ushike maagizo yako na kuyatii kwa uaminifu mpaka siku ile atakapotokea Bwana wetu Yesu Kristo.
15 Kutokea kwake kutafanyika wakati ufaao uliopangwa na Mungu mwenye heri na aliye Mtawala pekee, Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana.
16 Yeye peke yake anaishi milele katika mwanga usioweza kukaribiwa na mtu. Hakuna mtu aliyepata kumwona au awezaye kumwona. Kwake iwe heshima na uwezo wa milele! Amina.
17 Waamuru watu walio matajiri katika mambo ya maisha ya sasa, wasijivune, wasiweke tumaini lao katika mali isiyoweza kutegemewa; bali wamtegemee Mungu, ambaye kwa ukarimu hutupatia vitu vyote tuvifurahie.
18 Waamuru watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, na wawe wakarimu na walio tayari kuwashirikisha wengine mali zao.
19 Kwa namna hiyo watajiwekea hazina ambayo itakuwa kwao msingi imara kwa wakati ujao. Hapo wataweza kujipatia uhai ambao ni uhai wa kweli.