5 Mwenye upendo hakosi adabu, hatafuti faida yake binafsi, wala hana wepesi wa hasira; haweki kumbukumbu ya mabaya,
6 hafurahii uovu, bali hufurahia ukweli.
7 Mwenye upendo huvumilia yote, huamini yote, na hustahimili yote.
8 Upendo hauna kikomo kamwe. Kama kuna vipaji vya kutangaza ujumbe wa Mungu, hivyo vitatoweka siku moja; kama ni vipaji vya kusema lugha ngeni, vitakoma; kama kuna elimu, nayo itapita.
9 Maana ujuzi wetu si kamili, na kipaji chetu cha kutangaza neno la Mungu si kamili.
10 Lakini kile kilicho kikamilifu kitakapofika, vyote visivyo vikamilifu vitatoweka.
11 Nilipokuwa mtoto mchanga nilisema kitoto, nilifahamu kitoto, nilifikiri kitoto. Lakini sasa, maadamu mimi ni mtu mzima, mambo ya kitoto nimeyaacha.