1 Mimi Simoni Petro, mtumishi na mtume wa Yesu Kristo, nawaandikia nyinyi ambao, kwa wema wake Mungu wetu na Mwokozi Yesu Kristo, mmejaliwa imani ileile ya thamani kuu tuliyojaliwa sisi.
2 Nawatakieni neema na amani tele katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu.
3 Kwa uwezo wake wa kimungu, Mungu ametujalia mambo yote tunayohitaji ili tuishi maisha ya kumcha Mungu kwa kumjua yeye aliyetuita tuushiriki utukufu na wema wake yeye mwenyewe.
4 Kwa namna hiyo ametujalia zawadi kuu na za thamani ambazo alituahidia, ili kwa zawadi hizo mpate kuziepa kabisa tamaa mbaya zilizomo duniani, na kuishiriki hali yake ya kimungu.