2 Tumeyaacha kabisa mambo yote ya aibu na ya kisirisiri. Hatuishi tena kwa udanganyifu, wala kwa kulipotosha neno la Mungu; bali kwa kuudhihirisha ukweli twajiweka chini ya uamuzi wa dhamiri za watu mbele ya Mungu.
3 Maana, kama Habari Njema tunayohubiri imefichika, imefichika tu kwa wale wanaopotea.
4 Hao hawaamini kwa sababu yule mungu wa ulimwengu huu amezitia giza akili zao wasipate kuuona wazi mwanga wa Habari Njema ya utukufu wa Kristo, ambaye ni mfano kamili wa Mungu.
5 Maana hatujitangazi sisi wenyewe, ila tunamhubiri Yesu Kristo aliye Bwana, sisi wenyewe tukiwa watumishi wenu kwa ajili ya Yesu.
6 Mungu ambaye alisema, “Mwanga na uangaze kutoka gizani,” ndiye mwenye kuiangaza mioyo yetu, na kutupatia mwanga wa ujuzi wa utukufu wa Mungu uangazao katika uso wa Kristo.
7 Basi, sisi tulio na hazina hii tuko tu kama vyombo vya udongo, ili ionekane wazi kwamba nguvu hiyo kuu yatoka kwa Mungu wala si kwetu sisi wenyewe.
8 Daima twapata taabu, lakini hatugandamizwi; twapata mashaka, lakini hatukati tamaa;