2 Wakorintho 11 BHN

Paulo na mitume wa uongo

1 Laiti mngenivumilia kidogo, hata kama mimi ni mjinga kiasi! Naam, nivumilieni kidogo.

2 Ninawaoneeni wivu lakini ni wivu wa Mungu; maana nyinyi ni kama bikira safi niliyemposa kwa mwanamume mmoja tu ambaye ndiye Kristo.

3 Lakini naogopa kwamba, kama vile yule nyoka kwa hila zake za uongo alimdanganya Hawa, fikira zenu zaweza kupotoshwa, mkauacha uaminifu wenu wa kweli kwa Kristo.

4 Maana mtu yeyote ajaye na kumhubiri Yesu aliye tofauti na yule tuliyemhubiri, nyinyi mwampokea kwa mikono miwili; au mnakubali roho au Injili tofauti kabisa na ile mliyopokea kutoka kwetu!

5 Sidhani kwamba mimi ni mdogo kuliko hao “mitume wakuu.”

6 Labda sina ufasaha wa lugha, lakini elimu ninayo; jambo hili tumelionesha wazi kwenu, kila mahali na kila wakati.

7 Mimi niliihubiri kwenu Habari Njema ya Mungu bila kudai mshahara; nilijinyenyekesha ili nipate kuwakweza nyinyi. Je, nilifanya vibaya?

8 Nilipofanya kazi kati yenu, mahitaji yangu yaligharimiwa na makanisa mengine. Kwa namna moja au nyingine niliwapokonya wao mali yao nipate kuwatumikia nyinyi.

9 Nilipokuwa nanyi sikumsumbua mtu yeyote nilipohitaji fedha; ndugu waliotoka Makedonia waliniletea kila kitu nilichohitaji. Nilikuwa mwangalifu sana nisiwe mzigo kwa namna yoyote ile, na nitaendelea kufanya hivyo.

10 Naahidi kwa ule ukweli wa Kristo ulio ndani yangu, kwamba hakuna kitakachoweza kunizuia kujivunia jambo hilo popote katika Akaya.

11 Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu eti siwapendi nyinyi? Mungu anajua kwamba nawapenda!

12 Nitaendelea kufanya kama ninavyofanya sasa, ili nisiwape nafasi wale wanaotafuta nafasi, nafasi ya kujivuna kwamba eti wanafanya kazi kama sisi.

13 Maana, hao ni mitume wa uongo, wafanyakazi wadanganyifu wanaojisingizia kuwa mitume wa Kristo.

14 Wala si ajabu, maana hata Shetani mwenyewe hujisingizia kuwa malaika wa mwanga!

15 Kwa hiyo si jambo la kushangaza ikiwa na hao watumishi wake wanajisingizia kuwa watumishi wa haki. Mwisho wao watapata kile wanachostahili kufuatana na matendo yao.

Mateso ya Paulo kama mtume

16 Tena nasema: Mtu asinifikirie kuwa mpumbavu. Lakini kama mkifikiri hivyo, basi, nichukueni kama mpumbavu ili nami nipate kuwa na cha kujivunia angaa kidogo.

17 Ninachosema sasa si kile alichoniagiza Bwana; kuhusu jambo hili la kujivuna, nasema tu kama mtu mpumbavu.

18 Maadamu wengi hujivuna kwa sababu za kidunia, nami pia nitajivuna.

19 Nyinyi ni wenye busara, ndiyo maana hata mnawavumilia wapumbavu!

20 Mnamvumilia hata mtu anayewafanya nyinyi watumwa, mtu mwenye kuwanyonya, mwenye kuwakandamiza, mwenye kuwadharau na kuwapiga usoni!

21 Kwa aibu nakubali kwamba sisi tulikuwa dhaifu.Iwe iwavyo, lakini kama kuna mtu yeyote anayethubutu kujivunia kitu – nasema kama mtu mpumbavu – mimi nathubutu pia.

22 Je, wao ni Waebrania? Hata mimi. Je, wao ni Waisraeli? Hata mimi. Wao ni wazawa wa Abrahamu? Hata mimi.

23 Wao ni watumishi wa Kristo? Hata mimi – nanena hayo kiwazimu – ni mtumishi wa Kristo zaidi kuliko wao. Mimi nimefanya kazi ngumu zaidi, nimekaa gerezani mara nyingi zaidi, nimepigwa mara nyingi zaidi na nimekaribia kifo mara nyingi.

24 Mara tano nilichapwa vile viboko arubaini kasoro kimoja vya Wayahudi.

25 Nilipigwa fimbo mara tatu, nilipigwa mawe mara moja; mara tatu nilivunjikiwa meli baharini, na humo nikakesha usiku kucha na kushinda mchana kutwa.

26 Kila mara safarini nimekabiliwa na hatari za mafuriko ya mito, na hatari za wanyama; hatari kutoka kwa wananchi wenzangu na kutoka kwa watu wa mataifa mengine; hatari za mjini, hatari za porini, hatari za baharini, hatari kutoka kwa ndugu wa uongo.

27 Nimefanya kazi na kutaabika, nimekesha bila usingizi mara nyingi; nimekuwa na njaa na kiu; mara nyingi nimefunga na kukaa katika baridi bila nguo.

28 Na, licha ya mengine mengi, kila siku nakabiliwa na shughuli za makanisa yote.

29 Kama mtu yeyote ni dhaifu, nami pia ni dhaifu; mtu yeyote akikwazwa, nami pia huwa na wasiwasi.

30 Ikinilazimu kujivuna, basi, nitajivunia udhaifu wangu.

31 Mungu na Baba wa Bwana Yesu – jina lake litukuzwe milele – yeye anajua kwamba sisemi uongo.

32 Nilipokuwa Damasko, mkuu wa mkoa, aliyekuwa chini ya mfalme Areta, alikuwa akiulinda mji wa Damasko ili anikamate.

33 Lakini, ndani ya kapu kubwa, niliteremshwa nje kupitia katika nafasi ukutani, nikachopoka mikononi mwake.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13