22 Kisha akasema, “Baba yangu amenikabidhi vitu vyote. Hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana atapenda kumfunulia.”
23 Halafu akawaelekea wafuasi wake akawaambia, “Heri wanaoona yale mnayoyaona nyinyi!
24 Hakika, manabii na wafalme walitamani kuona yale mnayoyaona nyinyi wasiyaone, na kusikia yale mnayoyasikia wasiyasikie.”
25 Baadaye mwanasheria mmoja alisimama, akamwuliza akitaka kumtega, “Mwalimu, nifanye nini ili nipate uhai wa milele?”
26 Yeye akamwuliza, “Imeandikwa nini katika sheria? Unaelewaje?”
27 Akamjibu, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote. Na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.”
28 Yesu akamwambia, “Vema! Fanya hivyo, nawe utaishi.”