Luka 6 BHN

Suala juu ya siku ya Sabato

1 Siku moja ya Sabato, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano, na wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke ya ngano, wakaondoa punje zake kwa mikono, wakala.

2 Baadhi ya Mafarisayo wakawauliza, “Mbona mnafanya jambo ambalo si halali siku ya Sabato?”

3 Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma jinsi alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa?

4 Yeye aliingia katika nyumba ya Mungu, akachukua ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu, akala na kuwapa wenzake. Haikuruhusiwa mtu kula mikate hiyo isipokuwa tu makuhani.”

5 Hivyo akawaambia, “Mwana wa Mtu ana uwezo juu ya Sabato.”

Mtu mwenye mkono uliopooza

6 Siku nyingine ya Sabato, Yesu aliingia katika sunagogi, akafundisha. Mle ndani kulikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kulia ulikuwa umepooza.

7 Waalimu wa sheria na Mafarisayo walitaka kupata kisa cha kumshtaki Yesu na hivyo wakawa wanangojea waone kama angemponya mtu siku ya Sabato.

8 Lakini Yesu alijua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Inuka, simama katikati.” Yule mtu akaenda kusimama katikati.

9 Kisha Yesu akawaambia, “Nawaulizeni, je, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuyaangamiza?”

10 Baada ya kuwatazama wote waliokuwa pale, akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako.” Naye akafanya hivyo, na mkono wake ukawa mzima tena.

11 Lakini wao wakakasirika sana, wakajadiliana jinsi ya kumtendea Yesu maovu.

Yesu anateua mitume kumi na wawili

12 Siku moja Yesu alikwenda mlimani kusali, akakesha huko usiku kucha akisali.

13 Kesho yake aliwaita wanafunzi wake, na miongoni mwao akawachagua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume:

14 Simoni (ambaye Yesu alimpa jina Petro) na Andrea ndugu yake, Yakobo na Yohane, Filipo na Bartholomayo,

15 Mathayo na Thoma, Yakobo wa Alfayo na Simoni (aliyeitwa Zelote),

16 Yuda wa Yakobo na Yuda Iskarioti ambaye baadaye alikuwa msaliti.

Yesu anafundisha na kuwaponya watu

17 Baada ya kushuka mlimani pamoja nao, Yesu alisimama mahali palipokuwa tambarare. Hapo kulikuwa na kundi kubwa la wanafunzi wake na umati wa watu waliotoka pande zote za Yudea na Yerusalemu na pwani ya Tiro na Sidoni. Wote walifika kumsikiliza Yesu na kuponywa magonjwa yao.

18 Aliwaponya pia wote waliokuwa wanasumbuliwa na pepo wachafu.

19 Watu wote walitaka kumgusa, kwa maana nguvu ilikuwa inatoka ndani yake na kuwaponya wote.

Heri na ole

20 Yesu akawageukia wanafunzi wake, akasema:“Heri nyinyi mlio maskini,maana ufalme wa Mungu ni wenu.

21 Heri nyinyi mnaosikia njaa sasa,maana baadaye mtashiba.Heri nyinyi mnaolia sasa,maana baadaye mtacheka kwa furaha.

22 “Heri yenu nyinyi iwapo watu watawachukia, watawatenga, watawatukana na kuwaharibieni jina kwa ajili ya Mwana wa Mtu.

23 Wakati hayo yatakapotokea, furahini na kucheza, maana hakika tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Kwa maana wazee wao waliwatendea manabii vivyo hivyo.

24 Lakini ole wenu nyinyi mlio matajiri,maana mmekwisha pata faraja yenu.

25 Ole wenu nyinyi mnaoshiba sasa,maana baadaye mtasikia njaa.Ole wenu nyinyi mnaocheka kwa furaha sasa,maana baadaye mtaomboleza na kulia.

26 Ole wenu nyinyi iwapo watu wote wanawasifu,maana wazee wao waliwafanyia manabii wa uongo vivyo hivyo.

Kuwapenda maadui

27 “Lakini nawaambieni nyinyi mnaonisikiliza, wapendeni maadui zenu, watendeeni mema wale wanaowachukieni.

28 Watakieni baraka wale wanaowalaani, na waombeeni wale wanaowatendea vibaya.

29 Mtu akikupiga shavu moja mgeuzie pia la pili. Mtu akikunyanganya koti lako mwachie pia shati lako.

30 Yeyote anayekuomba mpe, na mtu akikunyanganya mali yako usimtake akurudishie.

31 Jinsi mnavyotaka watu wawatendee nyinyi, watendeeni wao vivyo hivyo.

32 “Na ikiwa mnawapenda tu wale wanaowapenda nyinyi, je, mtapata tuzo gani? Hakuna! Kwa maana hata wenye dhambi huwapenda wale wanaowapenda wao.

33 Tena, kama mkiwatendea mema wale tu wanaowatendeeni mema, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi hufanya hayo.

34 Na kama mnawakopesha wale tu mnaotumaini watawalipeni, je, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi wenzao ili warudishiwe kima kilekile.

35 Ila nyinyi wapendeni maadui zenu na kuwatendea mema; kopesheni bila kutazamia kurudishiwa, na tuzo lenu litakuwa kubwa, nanyi mtakuwa watoto wa Mungu aliye juu. Kwa maana yeye ni mwema kwa wale wasio na shukrani na walio wabaya.

36 Muwe na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma.

Juu ya kuwahukumu wengine

37 “Msiwahukumu wengine, nanyi hamtahukumiwa; msiwalaumu wengine, nanyi hamtalaumiwa; wasameheni wengine, nanyi mtasamehewa.

38 Wapeni wengine wanavyohitaji, nanyi mtapewa. Naam, mtapokea mikononi mwenu kipimo kilichojaa, kikashindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika. Kwa maana kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho atakachotumia Mungu kwenu.”

39 Akawaambia mfano huu: “Je, kipofu anaweza kumwongoza kipofu mwenzake? La! Wote wataanguka shimoni.

40 Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, lakini kila mwanafunzi akisha hitimu huwa kama mwalimu wake.

41 Kwa nini wakiona kibanzi jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti iliyoko jichoni mwako?

42 Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako,’ na huku huioni boriti iliyomo katika jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe! Toa kwanza boriti iliyomko jichoni mwako, na hapo ndipo utaona sawasawa kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako.

Mtu hujulikana kwa matunda yake

43 “Mti mzuri hauzai matunda mabaya, wala mti mbaya hauzai matunda mazuri.

44 Watu huutambua mti kutokana na matunda yake. Ni wazi kwamba watu hawachumi tini katika michongoma, wala hawachumi zabibu katika mbigili.

45 Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka katika hazina bora iliyomo moyoni mwake; na mtu mbaya hutoa yaliyo mabaya kutoka katika hazina mbaya iliyo moyoni mwake, kwa maana mtu huongea kutokana na yale yaliyojaa moyoni mwake.

Wajenzi wa namna mbili

46 “Mbona mwaniita ‘Bwana, Bwana,’ na huku hamtimizi yale ninayosema?

47 Nitawapeni mfano unaofaa kuonesha alivyo yeyote yule anayekuja kwangu, akasikia maneno yangu na kuyatimiza:

48 Huyo anafanana na mtu ajengaye nyumba, ambaye amechimba chini na kuweka msingi wake juu ya mwamba; kukatokea mafuriko ya mto, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, lakini haukuweza kuitikisa, kwa sababu ilikuwa imejengwa imara.

49 Lakini yeyote anayesikia maneno yangu asifanye chochote, huyo anafanana na mtu aliyejenga nyumba juu ya udongo, bila msingi. Mafuriko ya mto yakatokea, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, ikaanguka na kuharibika kabisa!”

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24