17 Tajiri huyo akafikiri moyoni mwake: ‘Nitafanyaje nami sina mahali pa kuhifadhia mavuno yangu?
18 Nitafanya hivi: Nitabomoa ghala zangu na kujenga kubwa zaidi, nami nitahifadhi humo mavuno yangu yote na mali yangu.
19 Hapo nitaweza kuiambia roho yangu: Sasa unayo akiba ya matumizi kwa miaka na miaka. Ponda mali, kula, kunywa na kufurahi.’
20 Lakini Mungu akamwambia: ‘Mpumbavu wewe; leo usiku roho yako itachukuliwa. Na vitu vile vyote ulivyojirundikia vitakuwa vya nani?’”
21 Yesu akamaliza kwa kusema, “Ndivyo ilivyo kwa mtu anayejirundikia mali kwa ajili yake mwenyewe, lakini si tajiri mbele ya Mungu.”
22 Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa sababu hiyo nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula mnachohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu.
23 Kwa sababu uzima ni bora kuliko chakula, na mwili ni bora kuliko mavazi.