1 Yesu aliingia mjini Yeriko, akawa akipita katika njia za mji huo.
2 Palikuwa na mtu mmoja huko mjini aitwaye Zakayo ambaye alikuwa mkuu wa watozaushuru, na pia mtu tajiri.
3 Alitaka kuona Yesu alikuwa nani, lakini kwa sababu ya umati wa watu, na kwa vile alikuwa mfupi, hakufaulu.
4 Hivyo, alitangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu ili aweze kumwona Yesu, kwa maana alikuwa apitie hapo.
5 Basi, Yesu alipofika mahali pale, aliangalia juu akamwambia, “Zakayo, shuka upesi, maana leo ni lazima nishinde nyumbani mwako.”
6 Zakayo akashuka haraka, akamkaribisha kwa furaha.
7 Watu wote walipoona hayo, wakaanza kunungunika wakisema, “Amekwenda kukaa kwa mtu mwenye dhambi.”