46 Yesu akalia kwa sauti kubwa: “Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.” Alipokwisha sema hayo, akakata roho.
47 Hapo, yule jemadari alipoona yaliyotukia akamsifu Mungu akisema: “Hakika huyu alikuwa mtu mwema.”
48 Watu wale wote waliokuwa wamekusanyika hapo kwa ajili ya tukio hilo, walipoona hayo yaliyotukia, walirudi makwao wakijipiga vifua kwa huzuni.
49 Marafiki zake wote pamoja na wale wanawake walioandamana naye kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali kutazama tukio hilo.
50 Kulikuwa na mtu mmoja jina lake Yosefu, mwenyeji wa kijiji kimoja cha Wayahudi kiitwacho Arimathaya. Alikuwa mtu mwema anayeheshimika.
51 Alikuwa akitazamia kuja kwa ufalme wa Mungu. Ingawa alikuwa mmoja wa Baraza Kuu la Wayahudi, hakuwa amekubaliana nao katika kitendo chao.
52 Basi, yeye alikwenda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu.