6 Hayuko hapa; amefufuka. Kumbukeni aliyowaambieni alipokuwa kule Galilaya:
7 ‘Ni lazima Mwana wa Mtu atolewe kwa watu waovu, nao watamsulubisha na siku ya tatu atafufuka.’”
8 Hapo hao wanawake wakayakumbuka maneno yake,
9 wakarudi kutoka kaburini, wakawapa mitume wale kumi na mmoja na wafuasi wengine habari za mambo hayo yote.
10 Hao waliotoa habari hizo kwa mitume ni: Maria Magdalene, Yoana na Maria mama wa Yakobo, pamoja na wanawake wengine walioandamana nao.
11 Mitume waliyachukua maneno hayo kama yasiyo na msingi, hivyo hawakuamini.
12 Lakini Petro alitoka, akaenda mbio hadi kaburini. Alipoinama kuchungulia ndani, akaiona tu ile sanda. Akarudi nyumbani huku akiwa anashangaa juu ya hayo yaliyotokea.