31 Kisha Yesu akashuka mpaka Kafarnaumu wilayani Galilaya, akawa anawafundisha watu siku ya Sabato.
32 Wakastaajabia uwezo aliokuwa nao katika kufundisha.
33 Na katika lile sunagogi kulikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu; akapiga ukelele wa kuziba masikio:
34 “Una nini nasi, wewe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakufahamu wewe ni nani. Wewe ni Mtakatifu wa Mungu!”
35 Yesu akamkemea huyo pepo akisema: “Nyamaza! Mtoke mtu huyu!” Basi, huyo pepo baada ya kumwangusha yule mtu chini, akamtoka bila kumdhuru hata kidogo.
36 Watu wote wakashangaa, wakawa wanaambiana, “Hili ni jambo la ajabu, maana kwa uwezo na nguvu anawaamuru pepo wachafu watoke, nao wanatoka!”
37 Habari za Yesu zikaenea mahali pote katika eneo lile.