2 Halafu akawatuma waende kuhubiri ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa.
3 Akawaambia, “Mnaposafiri msichukue chochote: Msichukue fimbo, wala mkoba, wala chakula, wala fedha, wala hata koti la ziada.
4 Nyumba yoyote mtakayoingia na kukaribishwa, kaeni humo mpaka mtakapoondoka katika kijiji hicho.
5 Watu wakikataa kuwakaribisha, tokeni katika mji huo, nanyi mnapotoka kunguteni mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao.”
6 Basi, wakaanza safari, wakapitia vijijini wakihubiri Habari Njema na kuponya wagonjwa kila mahali.
7 Sasa, mtawala Herode alipata habari za mambo yote yaliyokuwa yanatendeka, akawa na wasiwasi kwa vile walikuwa wakisema: “Yohane amefufuka kutoka kwa wafu!”
8 Wengine walisema kwamba Elia ametokea, na wengine walisema kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amerudi duniani.