1 Yesu alipokuwa anatoka hekaluni mmoja wa wanafunzi wake alimwambia, “Mwalimu, tazama jinsi mawe haya na majengo haya yalivyo ya ajabu!”
2 Yesu akamwambia, “Je, unayaona majengo haya makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitabomolewa.”
3 Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni akielekea hekalu, Petro, Yakobo, Yohane na Andrea wakamwuliza kwa faragha,
4 “Tuambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonesha kwamba mambo haya karibu yatimizwe?”
5 Yesu akaanza kuwaambia, “Jihadharini msije mkadanganywa na mtu.
6 Maana wengi watakuja wakilitumia jina langu, kila mmoja akisema kuwa yeye ni mimi! Nao watawapotosha watu wengi.