1 Ilikuwa siku mbili tu kabla ya sikukuu ya Pasaka na ya mikate isiyotiwa chachu. Makuhani wakuu na waalimu wa sheria walikuwa wakitafuta njia ya kumtia Yesu nguvuni kwa hila, wamuue.
2 Lakini walisema, “Tusimtie nguvuni wakati wa sikukuu, watu wasije wakafanya ghasia.”
3 Yesu alikuwa Bethania, nyumbani kwa Simoni Mkoma. Alipokuwa mezani kula chakula, mama mmoja aliyekuwa na chupa ya alabasta yenye marashi ya nardo safi ya thamani kubwa alikuja, akaivunja hiyo chupa, akammiminia Yesu marashi hayo kichwani.
4 Baadhi ya watu waliokuwa hapo walikasirika, wakajisemea, “Kwa nini kupoteza ovyo marashi haya?