34 Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.”
35 Yesu alipokuwa bado anaongea, watu walifika kutoka nyumbani kwa yule ofisa wa sunagogi, wakamwambia, “Binti yako amekwisha kufa. Ya nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?”
36 Lakini, bila kujali walichosema, Yesu akamwambia mkuu wa sunagogi, “Usiogope, amini tu.”
37 Wala hakumruhusu mtu yeyote kufuatana naye ila Petro, Yakobo na Yohane nduguye Yakobo.
38 Wakafika nyumbani kwa ofisa wa sunagogi naye Yesu akasikia makelele, kilio na maombolezo mengi.
39 Akaingia ndani, akawaambia, “Mbona mnapiga kelele na kulia? Msichana hakufa, amelala tu.”
40 Lakini wao wakamcheka. Basi, akawatoa wote nje, akawachukua baba yake na mama yake huyo msichana na wale wanafunzi wake, wakaingia chumbani alimokuwa huyo msichana.