25 Hapo mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo, alisikia habari za Yesu. Basi, akaja akajitupa chini mbele ya miguu yake.
26 Mama huyo alikuwa Mgiriki, mwenyeji wa Sirofoinike. Basi, akamwomba Yesu amtoe binti yake pepo mchafu.
27 Yesu akamwambia, “Kwanza watoto washibe; kwa maana si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”
28 Lakini huyo mama akasema, “Ni kweli, Bwana; lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto.”
29 Yesu akamwambia, “Kwa sababu ya neno hilo, nenda. Pepo amemtoka binti yako!”
30 Basi, akaenda nyumbani kwake, akamkuta mtoto amelala kitandani, na pepo amekwisha mtoka.
31 Kisha Yesu aliondoka wilaya ya Tiro, akapitia Sidoni, akafika ziwa Galilaya kwa kupitia nchi ya Dekapoli.