17 Hapo mtu mmoja katika ule umati wa watu akamjibu, “Mwalimu, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo aliyemfanya kuwa bubu.
18 Kila mara anapomvamia, humwangusha chini na kumfanya atokwe na povu kinywani, akisaga meno na kuwa mkavu mwili wote. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo lakini hawakuweza.”
19 Yesu akawaambia, “Enyi kizazi kisicho na imani! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni kwangu.”
20 Wakampeleka. Mara tu huyo pepo alipomwona Yesu, alimtia mtoto kifafa, naye mtoto akaanguka chini, akagaagaa na kutoka povu kinywani. Yesu akamwuliza baba yake huyo mtoto,
21 “Amepatwa na mambo hayo tangu lini?” Naye akamjibu, “Tangu utoto wake.
22 Na mara nyingi pepo huyo amemwangusha motoni na majini, ili amwangamize kabisa. Basi, ikiwa waweza, utuhurumie na kutusaidia!”
23 Yesu akamwambia, “Ati ikiwa waweza! Mambo yote yanawezekana kwa mtu aliye na imani.”