11 Mungu alifanya miujiza ya ajabu kwa mikono ya Paulo.
12 Watu walikuwa wakichukua leso na nguo nyingine za kazi ambazo Paulo alikuwa amezitumia, wakazipeleka kwa wagonjwa, nao wakaponywa magonjwa yao; na wale waliokuwa na pepo wabaya wakatokwa na pepo hao.
13 Wayahudi kadhaa wenye kupunga pepo wabaya walisafiri huko na huko wakijaribu kulitumia jina la Bwana Yesu kwa wale waliokuwa wamepagawa na pepo wabaya. Walikuwa wakisema: “Ninawaamuru kwa jina la Yesu ambaye Paulo anamhubiri.”
14 Watoto saba wa Skewa, kuhani mkuu wa Kiyahudi, walikuwa miongoni mwa hao waliokuwa wanafanya hivyo.
15 Lakini pepo mbaya aliwajibu, “Ninamfahamu Yesu, ninamjua pia Paulo, lakini nyinyi ni nani?”
16 Kisha yule mtu aliyepagawa aliwarukia wote kwa kishindo, akawashinda nguvu. Na hao watoto wa Skewa wakakimbia kutoka ile nyumba wakiwa uchi na wamejaa majeraha.
17 Kila mtu huko Efeso, Myahudi na asiye Myahudi, alisikia juu ya tukio hilo. Wote waliingiwa na hofu, wakalitukuza jina la Bwana Yesu.