15 Lakini pepo mbaya aliwajibu, “Ninamfahamu Yesu, ninamjua pia Paulo, lakini nyinyi ni nani?”
16 Kisha yule mtu aliyepagawa aliwarukia wote kwa kishindo, akawashinda nguvu. Na hao watoto wa Skewa wakakimbia kutoka ile nyumba wakiwa uchi na wamejaa majeraha.
17 Kila mtu huko Efeso, Myahudi na asiye Myahudi, alisikia juu ya tukio hilo. Wote waliingiwa na hofu, wakalitukuza jina la Bwana Yesu.
18 Waumini wengi walijitokeza wakakiri hadharani mambo waliyokuwa wametenda.
19 Wengine waliokuwa wameshughulikia mambo ya uchawi hapo awali, walikusanya vitabu vyao, wakavichoma mbele ya wote. Walikisia gharama ya vitabu hivyo, wakaona yafikia vipande 50,000 vya fedha.
20 Kwa namna hiyo, neno la Bwana lilizidi kuenea na kuwa na nguvu zaidi.
21 Baada ya mambo hayo, Paulo aliamua kwenda Yerusalemu kwa kupitia Makedonia na Akaya. Alisema, “Baada ya kufika huko, itanilazimu kuona Roma pia.”