4 Naye Paulo akasema, “Ubatizo wa Yohane ulikuwa wa kuonesha kwamba watu wametubu. Yohane aliwaambia watu wamwamini yule ambaye alikuwa anakuja baada yake, yaani Yesu.”
5 Baada ya kusikia hayo, walibatizwa kwa jina la Bwana Yesu.
6 Basi, Paulo akawawekea mikono, na Roho Mtakatifu akawashukia, wakaanza kusema lugha ngeni na kutangaza ujumbe wa Mungu.
7 Wote jumla walikuwa watu wapatao kumi na wawili.
8 Kwa muda wa miezi mitatu Paulo alikuwa akienda katika sunagogi, akawa na majadiliano ya kuvutia sana juu ya ufalme wa Mungu.
9 Lakini wengine walikuwa wakaidi, wakakataa kuamini, wakaanza kuongea vibaya juu ya hiyo njia ya Bwana katika kusanyiko la watu. Hapo Paulo alivunja uhusiano nao, akawachukua pembeni wale wanafunzi wake, akawa anazungumza nao kila siku katika jumba la masomo la Turano.
10 Aliendelea kufanya hivyo kwa muda wa miaka miwili hata wakazi wote wa Asia, Wayahudi na watu wa mataifa mengine, wakaweza kusikia neno la Bwana.