18 Walipofika kwake aliwaambia, “Mnajua jinsi nilivyokaa nanyi siku zote tangu siku ile ya kwanza nilipofika Asia.
19 Mnajua jinsi nilivyomtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, kwa machozi na matatizo yaliyonipata kutokana na mipango ya hila ya Wayahudi.
20 Mnajua kwamba sikusita hata kidogo kuwahubiria hadharani na nyumbani mwenu na kuwafundisha chochote ambacho kingewasaidieni.
21 Niliwaonya wote – Wayahudi, kadhalika na watu wa mataifa, wamgeukie Mungu na kumwamini Bwana wetu Yesu.
22 Sasa, sikilizeni! Mimi, nikiwa ninamtii Roho, nakwenda Yerusalemu bila kufahamu yatakayonipata huko.
23 Ninachojua tu ni kwamba Roho Mtakatifu ananithibitishia katika kila mji kwamba vifungo na mateso ndivyo vinavyoningojea.
24 Lakini, siuthamini uhai wangu kuwa kitu sana kwangu mradi tu nikamilishe ule utume wangu na ile kazi aliyonipa Bwana Yesu niifanye, yaani nishuhudie Habari Njema ya neema ya Mungu.