9 Watu wote waliokuwa hapo walimwona akitembea na kumsifu Mungu.
10 Walipomtambua kuwa ndiye yule aliyekuwa anaombaomba karibu na ule “Mlango Mzuri” wa hekalu, wakashangaa mno hata wasiweze kuelewa yaliyompata.
11 Watu wote, wakiwa na mshangao mkubwa, wakaanza kukimbilia mahali palipoitwa “Ukumbi wa Solomoni,” ambapo yule mtu alikuwa bado anaandamana na Petro na Yohane.
12 Basi, Petro alipowaona watu hao akawaambia, “Wananchi wa Israeli, kwa nini mnashangazwa na jambo hili? Mbona mnatukodolea macho kana kwamba ni kwa nguvu zetu au utakatifu wetu sisi wenyewe tumemfanya mtu huyu aweze kutembea?
13 Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo, Mungu wa babu zetu amemtukuza mtumishi wake Yesu. Yeye ndiye yuleyule mliyemtia mikononi mwa wakuu na kumkataa mbele ya Pilato hata baada ya Pilato kuamua kumwacha huru.
14 Alikuwa mtakatifu na mwema; lakini nyinyi mlimkataa, mkataka mtu mwingine aliyekuwa muuaji afunguliwe.
15 Basi, mlimuua yule ambaye ni chanzo cha uhai. Lakini Mungu alimfufua, na sisi ni mashahidi wa tukio hilo.