2 Naye Stefano akasema, “Ndugu zangu na akina baba, nisikilizeni! Mungu alimtokea babu yetu Abrahamu alipokuwa kule Mesopotamia kabla hajaenda kukaa kule Harani.
3 Mungu alimwambia: ‘Ondoka katika nchi yako; waache watu wa ukoo wako; nenda katika nchi nitakayokuonesha!’
4 Kwa hivyo, Abrahamu alihama nchi ya Kaldayo, akaenda kukaa Harani. Baada ya kifo cha baba yake, Mungu alimtoa tena Harani akaja kukaa katika nchi hii mnayokaa sasa.
5 Mungu hakumpa hata sehemu moja ya nchi hii iwe mali yake; hata hivyo, alimwahidi kumpa nchi hii iwe yake na ya wazawa wake, ingawaje wakati huu hakuwa na mtoto.
6 Mungu alimwambia hivi: ‘Wazawa wako watapelekwa katika nchi inayotawaliwa na watu wengine, na huko watafanywa watumwa na kutendewa vibaya kwa muda wa miaka 400.
7 Lakini mimi nitalihukumu taifa hilo litakalowafanya watumwa. Kisha nitawatoa katika nchi hiyo ili waje kuniabudu mahali hapa.’
8 Halafu Mungu akafanya naye agano ambalo tohara ni ishara yake. Hivyo, Abrahamu alimtahiri mtoto wake Isaka siku ya nane baada ya kuzaliwa. Na Isaka, vivyo hivyo, alimtahiri Yakobo. Naye Yakobo aliwatendea wale mababu kumi na wawili vivyo hivyo.