26 Kesho yake, aliwaona Waisraeli wawili wakipigana, akajaribu kuwapatanisha akisema: ‘Nyinyi ni ndugu; kwa nini basi, kutendeana vibaya nyinyi kwa nyinyi?’
27 Yule aliyekuwa anampiga mwenzake alimsukuma Mose kando akisema: ‘Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wetu?
28 Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri jana?’
29 Baada ya kusikia hayo, Mose alikimbia, akaenda kukaa katika nchi ya Midiani na huko akapata watoto wawili.
30 “Miaka arubaini ilipotimia, malaika wa Bwana alimtokea Mose katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto kule jangwani karibu na mlima Sinai.
31 Mose alistaajabu sana kuona tukio hilo hata akasogea karibu ili achungulie; lakini alisikia sauti ya Bwana:
32 ‘Mimi ni Mungu wa babu zako, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo!’ Mose akatetemeka kwa hofu na wala hakuthubutu kutazama zaidi.