21 Watu wote waliomsikia walishangaa, wakasema, “Je, mtu huyu si yuleyule aliyewaua wale waliokuwa wanaomba kwa jina hili kule Yerusalemu? Tena alikuja hapa akiwa na madhumuni ya kuwatia nguvuni watu hao na kuwapeleka kwa makuhani!”
22 Saulo alizidi kupata nguvu, na kwa jinsi alivyothibitisha wazi kwamba Yesu ndiye Kristo, Wayahudi wa huko Damasko walivurugika kabisa.
23 Baada ya siku nyingi kupita, Wayahudi walikusanyika na kufanya mpango wa kumuua Saulo.
24 Lakini Saulo alipata habari ya mpango huo. Usiku na mchana walilinda milango ya kuingia mjini ili wapate kumuua.
25 Lakini wakati wa usiku wanafunzi wake walimchukua, wakamteremsha chini ndani ya kapu kubwa kwa kupitia nafasi iliyokuwako ukutani.
26 Saulo alipofika Yerusalemu alijaribu kujiunga na wale wanafunzi. Lakini wote walimwogopa hawakuweza kuamini kwamba yeye amekuwa mfuasi.
27 Hapo, Barnaba alikuja akamchukua Saulo, akampeleka kwa mitume na kuwaeleza jinsi Saulo alivyomwona Bwana njiani na jinsi Bwana alivyoongea naye. Aliwaambia pia jinsi Saulo alivyokuwa amehubiri bila woga kule Damasko.