33 Huko alimkuta mtu mmoja aitwaye Ainea ambaye kwa muda wa miaka minane alikuwa amelala kitandani kwa sababu alikuwa amepooza.
34 Basi, Petro akamwambia, “Ainea, Yesu Kristo anakuponya. Amka utandike kitanda chako.” Ainea akaamka mara.
35 Wakazi wote wa Luda na Saroni walimwona Ainea, na wote wakamgeukia Bwana.
36 Kulikuwa na mfuasi mmoja mwanamke mjini Yopa aitwaye Tabitha (kwa Kigiriki ni Dorka, maana yake, Paa). Huyo mwanamke alikuwa akitenda mema na kuwasaidia maskini daima.
37 Wakati huo ikawa kwamba aliugua, akafa. Watu wakauosha mwili wake, wakaulaza katika chumba ghorofani.
38 Yopa si mbali sana na Luda; kwa hiyo wafuasi waliposikia kwamba Petro alikuwa Luda, wakawatuma watu wawili kwake na ujumbe: “Njoo kwetu haraka iwezekanavyo.”
39 Basi, Petro akaenda pamoja nao. Alipofika alipelekwa ghorofani katika kile chumba. Huko wajane wengi walimzunguka Petro wakilia na kumwonesha makoti na nguo ambazo Dorka alikuwa akitengeneza wakati alipokuwa hai.