1 Yesu alisema nao tena kwa kutumia mifano:
2 “Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme aliyemwandalia mwanawe karamu ya harusi.
3 Basi, akawatuma watumishi kuwaita walioalikwa waje harusini, lakini walioalikwa hawakutaka kufika.
4 Akawatuma tena watumishi wengine, akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa: Karamu yangu iko tayari sasa; fahali wangu na ndama wanono wamekwisha chinjwa; kila kitu ni tayari; njoni harusini.’
5 Lakini wao hawakujali, wakaenda zao; mmoja shambani kwake, mwingine kwenye shughuli zake,
6 na wengine wakawakamata wale watumishi wakawatukana, wakawaua.
7 Yule mfalme akakasirika, akawatuma askari wake wakawaangamize wauaji hao na kuuteketeza mji wao.