7 Tazama! Anakuja na mawingu!Kila mtu atamwona, na hata wale waliomtoboa.Makabila yote duniani yataomboleza juu yake.Naam! Amina.
8 “Mimi ni Alfa na Omega,” asema Bwana Mungu Mwenye Nguvu, aliyeko, aliyekuwako na anayekuja.
9 Mimi ni Yohane, ndugu yenu, ambaye kwa kuungana na Yesu, nashiriki pamoja nanyi mateso na ufalme wake na uvumilivu thabiti. Mimi nilikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo kwa sababu ya kuhubiri neno la Mungu na kumshuhudia Yesu.
10 Basi, wakati mmoja, siku ya Bwana, nilikumbwa na Roho, nikasikia nyuma yangu sauti kubwa kama sauti ya tarumbeta.
11 Nayo ilisema, “Andika katika kitabu yale unayoyaona, ukipeleke kwa makanisa haya saba: Efeso, Smurna, Pergamumu, Thuatira, Sarde, Filadelfia na Laodikea.”
12 Basi, nikageuka nimwone huyo aliyesema nami, nikaona vinara vya taa saba vya dhahabu,
13 na katikati yake kulikuwa na kitu kama Mwana wa Mtu, naye alikuwa amevaa kanzu ndefu na mkanda wa dhahabu kifuani.