1 Baada ya hayo nilitazama nikaona mlango umefunguliwa mbinguni. Na ile sauti niliyoisikia pale awali ambayo ilikuwa kama sauti ya tarumbeta, ikasema, “Njoo hapa juu, nami nitakuonesha mambo yatakayotukia baadaye.”
2 Mara nikakumbwa na Roho. Kumbe, huko mbinguni kuna kiti cha enzi na juu yake ameketi mmoja.
3 Huyo aliyeketi juu yake alikuwa kama almasi na jiwe zuri jekundu. Upinde wa mvua ulikuwa unang'aa kama zumaridi na ulikizunguka kiti cha enzi pande zote.
4 Kulikuwa na duara la viti ishirini na vinne kukizunguka kiti cha enzi, na juu ya viti hivyo wazee ishirini na wanne walikuwa wameketi wamevaa mavazi meupe na taji za dhahabu vichwani.
5 Umeme, sauti na ngurumo, vilikuwa vinatoka kwenye hicho kiti cha enzi. Taa saba za moto zilikuwa zinawaka mbele ya hicho kiti cha enzi. Taa hizo ni roho saba za Mungu.
6 Mbele ya kiti cha enzi kulikuwa na kitu kama bahari ya kioo, angavu kama jiwe ling'aalo sana.Katika pande zote za hicho kiti cha enzi na kukizunguka, kulikuwa na viumbe hai wanne. Viumbe hao walikuwa wamejaa macho mbele na nyuma.
7 Kiumbe wa kwanza alikuwa kama simba, wa pili kama ng'ombe, wa tatu alikuwa na sura ya mtu, na wa nne alikuwa kama tai anayeruka.
8 Viumbe hao wanne walikuwa na mabawa sita kila mmoja, na walikuwa wamejaa macho, ndani na nje. Usiku na mchana, bila kupumzika, huimba:“Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu,Bwana, Mungu Mwenye Nguvu,aliyekuwako, aliyeko na anayekuja!”
9 Kila mara viumbe hao wanne walipomtukuza na kumheshimu na kumshukuru huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi ambaye anaishi milele na milele,
10 wale wazee ishirini na wanne hujiangusha mbele ya huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi na kumwabudu huyo ambaye anaishi milele na milele; na huziweka taji zao mbele ya kiti cha enzi wakisema:
11 “Wastahili ee Bwana na Mungu wetu,kupokea utukufu na heshima na nguvu.Maana wewe uliumba vitu vyote,na kwa matakwa yako viliumbwa na vipo.”