23 Mnapaswa, lakini kuendelea na msingi imara katika imani, wala msikubali kutikiswa kutoka katika tumaini lile mlilopata wakati mlipoisikia Injili. Mimi Paulo nimekuwa mtumishi wa hiyo Injili ambayo imekwisha hubiriwa kila mtu duniani.
24 Na sasa nafurahi kuteseka kwa ajili yenu, maana kwa mateso yangu hapa duniani, nasaidia kukamilisha kile kilichopungua bado katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, yaani kanisa.
25 Nami nimefanywa kuwa mtumishi wa kanisa kufuatana na mpango wake Mungu ambao alinikabidhi kwa faida yenu. Mpango wenyewe ni kuutangaza kwa ukamilifu ujumbe wake,
26 ambao ni siri aliyowaficha binadamu wote tangu milele, lakini sasa amewajulisha watu wake.
27 Mungu ametaka kuwajulisha hao jinsi siri hiyo ilivyo kuu na tukufu ambayo imeenea kwa watu wa mataifa, nayo ndiyo hii: Kristo yuko ndani yenu, na jambo hilo lamaanisha kwamba nyinyi mtaushiriki utukufu wa Mungu.
28 Kwa sababu hiyo tunamhubiri Kristo kwa watu wote; tunawaonya na kuwafundisha wote kwa hekima yote, ili tuweze kumleta kila mmoja mbele ya Mungu akiwa amekomaa katika kuungana na Kristo.
29 Kwa madhumuni hayo mimi nafanya kazi na kujitahidi nikiitumia nguvu kuu ya Kristo ifanyayo kazi ndani yangu.