1 Kwa hiyo, ndugu zangu, maadamu Mungu ni mwenye huruma nyingi, nawasihi kwa moyo wote: Mtoleeni Mungu miili yenu kama tambiko iliyo hai, takatifu na yenye kupendeza. Hii ndiyo njia yenu halisi ya kumwabudu.
2 Msiige mitindo ya ulimwengu huu, bali Mungu afanye mabadiliko ndani yenu kwa kuzigeuza fikira zenu. Hapo ndipo mtakapoweza kuyajua mapenzi ya Mungu na kutambua jambo lililo jema, linalompendeza na kamilifu.
3 Kutokana na neema aliyonijalia Mungu, nawaambieni nyinyi nyote: Msijione kuwa ni kitu zaidi kuliko mnavyopaswa kuwa. Fikira zenu na ziwe na kiasi kadiri ya kipimo cha imani Mungu aliyomgawia kila mmoja.
4 Mwili una viungo vingi, kila kimoja na kazi yake.
5 Hali kadhalika ingawa sisi ni wengi, tu mwili mmoja kwa kuungana na Kristo, na kila mmoja ni kiungo cha mwenzake.
6 Basi, tunavyo vipaji mbalimbali kadiri ya neema tuliyopewa. Mwenye kipaji cha unabii na akitumie kadiri ya imani yake.
7 Mwenye kipaji cha utumishi na atumikie. Mwenye kipaji cha kufundisha na afundishe.