13 Wala msitoe hata sehemu moja ya miili yenu iwe chombo cha kutenda uovu na dhambi. Badala yake, jitoleeni nyinyi wenyewe kwa Mungu kama watu waliofufuliwa kutoka kwa wafu; toeni nafsi zenu zote kwa Mungu kwa ajili ya uadilifu.
14 Maana, dhambi haitawatawala tena, kwani hamko chini ya sheria, bali chini ya neema.
15 Basi, tuseme nini? Je, tutende dhambi ati kwa sababu hatuko chini ya sheria bali chini ya neema? Hata kidogo!
16 Mnajua kwamba mkijitolea nyinyi wenyewe kama watumwa na kumtii fulani, mnakuwa kweli watumwa wake mtu huyo – au watumwa wa dhambi na matokeo yake ni kifo, au wa utii na matokeo yake ni kufanywa kuwa waadilifu.
17 Ingawa mlikuwa watumwa wa dhambi zamani, sasa lakini – namshukuru Mungu – mmetii kwa moyo wote yale maazimio na mafundisho mliyopokea.
18 Mlikombolewa kutoka utumwa wa dhambi, mkawa watumwa wa uadilifu
19 (hapa natumia lugha ya kawaida ya watu kwa sababu ya udhaifu wenu wenyewe). Kama vile wakati fulani mlivyojitolea nyinyi wenyewe kutumikia uchafu na uhalifu kwa ajili ya uovu, vivyo hivyo sasa jitoleeni nafsi zenu wenyewe kutumikia uadilifu kwa ajili ya utakatifu.