8 Basi, ikiwa tumekufa pamoja na Kristo, tunaamini kwamba tutaishi pia pamoja naye.
9 Maana, tunajua kwamba Kristo amekwisha fufuliwa kutoka kwa wafu na hafi tena; kifo hakimtawali tena.
10 Hivyo, kwa kuwa alikufa – mara moja tu – dhambi haina nguvu tena juu yake; na sasa anaishi maisha yake katika umoja na Mungu.
11 Hali kadhalika nanyi lazima mjione kuwa mmekufa kuhusu dhambi, lakini kama mnaoishi katika umoja na Mungu kwa njia ya Kristo Yesu.
12 Kwa hiyo, dhambi isiitawale tena miili yenu ambayo hufa, na hivyo kuzitii tamaa zake.
13 Wala msitoe hata sehemu moja ya miili yenu iwe chombo cha kutenda uovu na dhambi. Badala yake, jitoleeni nyinyi wenyewe kwa Mungu kama watu waliofufuliwa kutoka kwa wafu; toeni nafsi zenu zote kwa Mungu kwa ajili ya uadilifu.
14 Maana, dhambi haitawatawala tena, kwani hamko chini ya sheria, bali chini ya neema.