9 Ndugu aliye maskini anapaswa kufurahi wakati Mungu anapomkweza,
10 naye tajiri anapaswa kufurahi anaposhushwa na Mungu. Maana tajiri atatoweka kama ua la porini.
11 Jua huchomoza na kwa joto lake kali hukausha mimea, nayo maua yake huanguka, na uzuri wake wote huharibika. Vivyo hivyo, tajiri ataangamizwa katika shughuli zake.
12 Heri mtu anayebaki mwaminifu katika majaribu, kwani akisha stahimili, atapewa tuzo la uhai ambalo Mungu aliwaahidi wale wanaompenda.
13 Kama mtu akijaribiwa, asiseme: “Ninajaribiwa na Mungu.” Maana Mungu hawezi kujaribiwa na uovu, wala yeye hamjaribu mtu yeyote.
14 Lakini mtu hujaribiwa anapovutwa na kunaswa na tamaa zake mbaya.
15 Tamaa ikiiva huzaa dhambi; nayo dhambi ikikomaa huzaa kifo.