1 Ilikuwa siku kabla ya sikukuu ya Pasaka. Yesu alijua kwamba saa yake ya kuondoka ulimwenguni na kwenda kwa Baba ilikuwa imefika. Alikuwa amewapenda daima watu wake walioko duniani; naam, aliwapenda mpaka mwisho!
2 Basi, Yesu na wanafunzi wake walikuwa wamekaa kula chakula cha jioni. Ibilisi alikwisha mtia Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti, nia ya kumsaliti Yesu.
3 Yesu alijua kwamba Baba alikuwa amemkabidhi kila kitu, na kwamba alikuwa ametoka kwa Mungu na anarudi kwa Mungu.
4 Basi, aliondoka mezani, akaweka kando vazi lake, akachukua kitambaa na kujifunga kiunoni.
5 Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwaosha wanafunzi wake miguu na kuipangusa kwa kile kitambaa alichojifungia.
6 Basi, akamfikia Simoni Petro; naye Petro akasema, “Bwana, wewe utaniosha miguu mimi?”