1 Baada ya hayo, Yesu alivuka ziwa Galilaya (au ziwa Tiberia).
2 Umati mkubwa wa watu ulimfuata kwa sababu watu hao walikuwa wameona ishara alizokuwa akifanya kwa kuwaponya wagonjwa.
3 Yesu alipanda mlimani, akaketi pamoja na wanafunzi wake.
4 Sikukuu ya Wayahudi iitwayo Pasaka ilikuwa imekaribia.
5 Basi, Yesu alipotazama na kuona umati wa watu ukija kwake, alimwambia Filipo, “Tununue wapi mikate ili watu hawa wapate kula?”
6 (Alisema hivyo kwa kumjaribu Filipo, kwani alijua mwenyewe atakalofanya.)
7 Filipo akamjibu, “Mikate ya fedha dinari 200 haiwatoshi watu hawa hata kama kila mmoja atapata kipande kidogo tu!”
8 Mmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia,
9 “Yupo hapa mtoto mmoja aliye na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili; lakini hivi vyatosha nini kwa watu wengi kama hawa?”
10 Yesu akasema, “Waketisheni watu.” Palikuwa na nyasi tele mahali hapo. Basi, watu wakaketi, jumla yapata wanaume 5,000.
11 Yesu akaitwaa ile mikate, akamshukuru Mungu, akawagawia watu waliokuwa wameketi; akafanya vivyo hivyo na wale samaki, kila mtu akapata kadiri alivyotaka.
12 Watu waliposhiba Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki visipotee.”
13 Basi, wakakusanya vipande vya mikate ya shayiri walivyobakiza wale watu waliokula, wakajaza vikapu kumi na viwili.
14 Watu walipoiona ishara hiyo aliyoifanya Yesu, wakasema, “Hakika huyu ndiye nabii anayekuja ulimwenguni.”
15 Yesu akajua kwamba watu walitaka kumchukua wamfanye mfalme, akaondoka tena, akaenda mlimani peke yake.
16 Ilipokuwa jioni wanafunzi wake waliteremka hadi ziwani,
17 wakapanda mashua ili wavuke kwenda Kafarnaumu. Giza lilikuwa limeingia, na Yesu alikuwa hajawafikia bado.
18 Ziwa likaanza kuchafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma.
19 Wanafunzi walipokuwa wamekwenda umbali wa kilomita tano au sita, walimwona Yesu akitembea juu ya maji, anakaribia mashua; wakaogopa sana.
20 Yesu akawaambia, “Ni mimi, msiogope!”
21 Basi wakataka kumchukua Yesu katika mashua; na mara mashua ikawasili nchi kavu walikokuwa wanakwenda.
22 Kesho yake umati wa watu wale waliobaki upande wa pili wa ziwa walitambua kwamba kulikuwa na mashua moja tu pale, na Yesu hakuingia katika mashua pamoja na wanafunzi wake, ila wanafunzi hao walikuwa wamekwenda zao peke yao.
23 Mashua nyingine kutoka Tiberia zilifika mahali hapo watu walipokula ile mikate, Bwana alipokwisha mshukuru Mungu.
24 Basi, hao watu walipogundua kwamba Yesu na wanafunzi wake hawakuwapo mahali hapo, walipanda mashua, wakaenda Kafarnaumu wakimtafuta.
25 Wale watu walipomkuta Yesu ngambo ya pili wa ziwa walimwuliza, “Mwalimu, ulifika lini hapa?”
26 Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, mnanitafuta si kwa kuwa mmeona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba.
27 Msikishughulikie chakula kiharibikacho; kishughulikieni chakula kidumucho kwa ajili ya uhai wa milele. Mwana wa Mtu ambaye Baba amemthibitisha atawapeni chakula hicho.”
28 Wao wakamwuliza, “Tufanye nini ili tuweze kuzitenda kazi za Mungu?”
29 Yesu akawajibu, “Hii ndiyo kazi anayotaka Mungu mwifanye: Kumwamini yule aliyemtuma.”
30 Hapo wakamwambia, “Utafanya ishara gani ili tuione tupate kukuamini? Utafanya kitu gani?
31 Wazee wetu walikula mana kule jangwani, kama yasemavyo Maandiko: ‘Aliwalisha mkate kutoka mbinguni.’”
32 Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, Mose hakuwapeni mkate kutoka mbinguni; Baba yangu ndiye awapaye nyinyi mkate wa kweli kutoka mbinguni.
33 Maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na aupaye ulimwengu uhai.”
34 Basi, wakamwambia, “Bwana, tupe daima mkate huo.”
35 Yesu akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uhai. Anayekuja kwangu hataona njaa; anayeniamini hataona kiu kamwe.
36 Lakini niliwaambieni kwamba ingawa mmeniona hamniamini.
37 Wote anaonipa Baba watakuja kwangu; nami kamwe sitamtupa nje yeyote anayekuja kwangu,
38 kwani nimeshuka kutoka mbinguni si kwa ajili ya kufanya matakwa yangu, ila kutimiza matakwa ya yule aliyenituma.
39 Na matakwa ya yule aliyenituma ndiyo haya: Nisimpoteze hata mmoja kati ya wale alionipa, ila niwafufue wote siku ya mwisho.
40 Maana anachotaka Baba yangu ndicho hiki: Kila amwonaye Mwana na kumwamini awe na uhai wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.”
41 Basi, Wayahudi wakaanza kunungunika kwa kuwa alisema: “Mimi ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni.”
42 Wakasema, “Je, huyu si mwana wa Yosefu? Tunamjua baba yake na mama yake! Basi, anawezaje kusema kwamba ameshuka kutoka mbinguni?”
43 Yesu akawaambia, “Acheni kunungunika nyinyi kwa nyinyi.
44 Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, Baba aliyenituma asipomvuta kwangu; nami nitamfufua mtu huyo siku ya mwisho.
45 Manabii wameandika: ‘Watu wote watafundishwa na Mungu.’ Kila mtu anayemsikia Baba na kujifunza kutoka kwake, huja kwangu.
46 Hii haina maana kwamba yupo mtu aliyemwona Baba, isipokuwa yule aliyetoka kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba.
47 Kweli, nawaambieni, anayeamini anao uhai wa milele.
48 Mimi ni mkate wa uhai.
49 Wazee wenu walikula mana kule jangwani, lakini walikufa.
50 Lakini huu ni mkate unaoshuka kutoka mbinguni ili yeyote atakayeula asife.
51 Mimi ni mkate hai ulioshuka kutoka mbinguni. Mtu yeyote akila mkate huu ataishi milele. Na mkate nitakaompa ni mwili wangu ninaoutoa kwa ajili ya uhai wa ulimwengu.”
52 Ndipo Wayahudi wakaanza kubishana kati yao: “Anawezaje huyu kutupa mwili wake, tule?”
53 Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, msipokula mwili wa Mwana wa Mtu na kunywa damu yake, hamtakuwa na uhai ndani yenu.
54 Anayekula mwili wangu na kunywa damu yangu anao uhai wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho.
55 Maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli.
56 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu, akaa ndani yangu, nami nakaa ndani yake.
57 Baba aliye hai alinituma, nami naishi kwa sababu yake; vivyo hivyo anilaye mimi ataishi pia kwa sababu yangu.
58 Basi, huu ndio mkate ulioshuka kutoka mbinguni; si kama mana waliyokula babu zenu, wakafa. Aulaye mkate huu atakuwa hai milele.”
59 Yesu alisema hayo alipokuwa akifundisha katika sunagogi kule Kafarnaumu.
60 Basi, wengi wa wafuasi wake waliposikia hayo, wakasema, “Haya ni mambo magumu! Nani awezaye kuyasikiliza?”
61 Yesu alijua bila kuambiwa na mtu kwamba wanafunzi wake walikuwa wananungunika juu ya jambo hilo, akawauliza, “Je, jambo hili linawafanya muwe na mashaka?
62 Itakuwaje basi, mtakapomwona Mwana wa Mtu akipanda kwenda kule alikokuwa kwanza?
63 Roho ndiyo iletayo uhai; mwili hauwezi kitu. Maneno niliyowaambia ni roho na uhai.
64 Hata hivyo, wako baadhi yenu wasioamini.” (Yesu alisema hivyo kwani alijua tangu mwanzo ni kina nani wasioamini, na pia ni nani atakayemsaliti).
65 Kisha akasema, “Ndiyo maana niliwaambieni kwamba hakuna awezaye kuja kwangu asipowezeshwa na Baba yangu.”
66 Kutokana na hayo, wengi wa wafuasi wake walirudi nyuma, wasiandamane naye tena.
67 Basi, Yesu akawauliza wale kumi na wawili, “Je, nanyi pia mwataka kwenda zenu?”
68 Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tutakwenda kwa nani? Wewe unayo maneno ya uhai wa milele.
69 Sisi tunaamini, na tunajua kwamba wewe ndiwe yule Mtakatifu wa Mungu”
70 Yesu akawaambia, “Je, sikuwachagua nyinyi kumi na wawili? Hata hivyo, mmoja wenu ni Ibilisi!”
71 Yesu alisema hayo juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti; maana huyu alikuwa ndiye atakayemsaliti, ingawa alikuwa mmoja wa wale kumi na wawili.