1 Daudi alipokaribia kufariki, alimwita mwanawe Solomoni, akampa wosia akisema,
2 “Mwanangu, kama ilivyo kawaida kwa viumbe vyote kufa, siku zangu zimekwisha. Uwe imara na hodari.
3 Timiza maagizo ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ufuate njia zake na kushika masharti yake, amri zake, hukumu zake na kuheshimu maamuzi yake kama ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, ili upate kufanikiwa katika kila ufanyalo na kokote uendako, pia
4 ili Mwenyezi-Mungu atimize ahadi yake aliyotoa aliponiambia kuwa, ikiwa wazawa wangu watatii amri zake na kumtumikia kwa uaminifu na kwa moyo wote, hakutakosekana mmoja wao kutawala Israeli nyakati zote.
5 “Zaidi ya hayo, unajua pia yale aliyonitendea Yoabu, mwana wa Seruya; jinsi alivyowatendea majemadari wawili wa majeshi ya Israeli, Abneri mwana wa Neri, na Amasa mwana wa Yetheri. Aliwaua wakati wa amani akitaka kulipiza kisasi kwa mauaji waliyofanya wakati wa vita. Aliwaua watu wasiokuwa na hatia, nami nikachukua lawama kwa ajili ya vitendo vyake ambavyo vimeniletea mateso.
6 Basi, wewe fanya kadiri ya hekima yako, ila tu usimwache afe kwa amani.