1 Basi, Rehoboamu akaenda Shekemu ambako Waisraeli wote walikuwa wamekusanyika ili kumtawaza awe mfalme.
2 Naye Yeroboamu mwana wa Nebati alipopata habari kuhusu tendo hilo (maana alikuwa bado Misri ambako alikwenda alipomkimbia Solomoni), alirudi kutoka Misri.
3 Lakini Waisraeli walituma ujumbe na kumwita. Kisha, yeye pamoja na jumuiya yote ya Israeli, walimwendea Rehoboamu, wakamwambia,
4 “Baba yako alitutwisha mzigo mzito. Basi, utupunguzie mzigo huo, nasi tutakutumikia.”
5 Naye Rehoboamu akawaambia, “Nendeni, mrudi kwangu kesho kutwa.” Basi, wakaondoka.
6 Baadaye Rehoboamu alitaka kujua maoni ya wazee ambao walikuwa washauri wa baba yake Solomoni, alipokuwa angali hai, akawauliza, “Je, mnanishauri niwape jibu gani watu hawa?”
7 Wazee hao wakamjibu, “Leo ukiwa mtumishi wa watu hawa, ukawatumikia na kuongea nao vizuri unapowajibu, hapo watakuwa watumishi wako daima.”
8 Lakini Rehoboamu alipuuza shauri la wazee; badala yake akashauriana na vijana wa rika lake ambao walikuwa washauri wake.
9 Basi, akawauliza, “Nyinyi mnatoa shauri gani ili tuweze kuwajibu watu hawa walioniambia niwapunguzie mzigo ambao baba yangu aliwatwika?”
10 Hao vijana wakamjibu, “Watu hao waliokuambia baba yako aliwatwika mzigo mzito, wakakuomba uwapunguzie mzigo huo, wewe waambie hivi: ‘Kidole changu kidogo ni kinene zaidi kuliko kiuno cha baba yangu.
11 Mzigo wa baba yangu ulikuwa mzito, lakini wangu utakuwa mzito zaidi. Baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa mijeledi yenye miiba.’”
12 Basi, siku ya tatu Yeroboamu pamoja na watu wote wakarudi kwa Rehoboamu kama alivyokuwa amewaagiza.
13 Mfalme akawajibu watu hao kwa ukali, akapuuza shauri alilopewa na wazee,
14 akafuata shauri la vijana wenzake, akawaambia, “Baba yangu aliwatwika mzigo mzito, lakini mimi nitaufanya kuwa mzito zaidi. Baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa mijeledi yenye miiba.”
15 Hivyo, mfalme hakuwajali watu kwa sababu jambo hili lilisababishwa na Mwenyezi-Mungu, ili atimize neno lake alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati, kwa njia ya Ahiya wa Shilo.
16 Lakini watu wote wa Israeli walipoona kwamba mfalme hakuwajali, walimwambia,“Hatuna uhusiano wowote na Daudi!Hatuna sehemu yetu kutoka kwa huyo mwana wa Yese.Rudini nyumbani, enyi watu wa Israeli!Itunze nyumba yako mwenyewe, ee Daudi.”Hivyo, watu wa Israeli wakarudi makwao.
17 Watu wa Israeli waliokuwa wanakaa katika miji ya Yuda, ndio hao tu waliobaki chini ya utawala wa Rehoboamu.
18 Mfalme Rehoboamu alipomtuma Adoramu, aliyekuwa mnyapara mkuu wa kazi za kulazimishwa, watu wote wa Israeli walimpiga mawe, wakamuua. Naye Rehoboamu alipanda haraka gari lake la kukokotwa, akakimbilia Yerusalemu.
19 Hivyo watu wa Israeli wamekuwa katika hali ya uasi dhidi ya ukoo wa Daudi mpaka leo.
20 Watu wote wa Israeli walipopata habari kwamba Yeroboamu alikuwa amerudi kutoka Misri, walimwita katika mkutano wa hadhara, wakamtawaza kuwa mfalme wa Israeli yote. Hakuna kabila lingine lililojiunga na ukoo wa Daudi isipokuwa tu kabila la Yuda.
21 Rehoboamu alipofika Yerusalemu, alikusanya askari stadi 180,000 wa makabila ya Yuda na Benyamini, apate kupigana na utawala wa Israeli, ili aurudishe utawala kwake yeye mwenyewe Rehoboamu, mwana wa Solomoni.
22 Lakini ujumbe wa Mungu ulimjia Shemaya, mtu wa Mungu:
23 “Mwambie Rehoboamu mwana wa Solomoni, mfalme wa Yuda, na watu wote wa kabila la Yuda na Benyamini na watu wengine,
24 kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: ‘Msiende, wala msipigane na ndugu zenu, watu wa Israeli. Rudini kila mtu nyumbani kwake, maana hayo yaliyotokea ni mpango wangu.’” Basi, wakaufuata ujumbe huu wa Mwenyezi-Mungu, wakarudi nyumbani tena, kama Mwenyezi-Mungu alivyoagiza.
25 Baadaye mfalme Yeroboamu akaujenga upya mji wa Shekemu kwenye mlima wa Efraimu; akakaa huko. Kisha akaenda akajenga mji wa Penueli.
26 Ndipo Yeroboamu akaanza kufikirifikiri: “Sasa ufalme utarudi kwa jamaa ya mfalme Daudi
27 kama watu hawa wataendelea kwenda kutambikia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu huko Yerusalemu. Mioyo yao itamgeukia bwana wao Rehoboamu mfalme wa Yuda, nao wataniua mimi.”
28 Basi, baada ya kushauriana na wengine, akatengeneza sanamu za ndama mbili za dhahabu. Kisha akawaambia watu, “Enyi watu wa Israeli, hii ndiyo miungu yenu iliyowatoa katika nchi ya Misri! Hakuna sababu ya kwenda Yerusalemu kutambikia huko.”
29 Akaweka sanamu moja ya ndama wa dhahabu mjini Betheli, na ya pili mjini Dani.
30 Tendo hili likawa dhambi, maana watu waliandamana kwenda kuzitambikia sanamu hizo huko Betheli na Dani.
31 Vilevile, Yeroboamu alijenga mahali pa kutambikia vilimani, akateua makuhani, watu ambao hawakuwa wa ukoo wa Lawi.
32 Yeroboamu pia aliamuru siku ya kumi na tano ya mwezi wa nane iwe sikukuu sawa na ile sikukuu iliyokuwa inafanyika huko Yuda. Alitoa tambiko kwenye madhabahu aliyotengeneza huko Betheli mbele ya zile sanamu za ndama alizozitengeneza, akaweka wale makuhani aliowateua wahudumu kila mahali pa kutolea tambiko alikotengeneza vilimani.
33 Siku hiyo ya kumi na tano ya mwezi wa nane, aliibuni yeye mwenyewe, naye akaenda Betheli kutambikia. Ndivyo alivyoiimarisha sikukuu hiyo aliyoiweka kwa ajili ya watu wa Israeli, naye mwenyewe akapanda kuiendea madhabahu, kufukiza ubani.