20 Watu wa Yuda na wa Israeli walikuwa wengi kama mchanga wa pwani, nao walikuwa wakila, wakinywa, na kufurahi.
21 Solomoni alitawala falme zote kuanzia mto Eufrate mpaka nchi ya Wafilisti, hadi mpakani na Misri. Mataifa yote yalimtumikia na kulipa kodi kwake wakati wote wa maisha yake.
22 Chakula alichohitaji Solomoni kwa siku moja, kilikuwa unga laini madebe 360, na unga wa kawaida madebe 720,
23 ng'ombe wanono kumi, na ng'ombe wa kundini ishirini, kondoo 100 pamoja na kulungu, paa, swala na kuku wanono.
24 Naam, nchi yote magharibi ya mto Eufrate: Kutoka Tifsa mpaka mji wa Gaza, ilikuwa chini ya utawala wake. Wafalme wote magharibi ya mto Eufrate walikuwa chini yake, na alikuwa na amani na nchi zote jirani.
25 Siku zote za utawala wake Solomoni, watu wa Yuda na watu wa Israeli, toka Dani mpaka Beer-sheba, walikaa salama, kila mtu kwenye miti yake ya mizabibu na mitini.
26 Solomoni alikuwa na vibanda 40,000 kwa ajili ya farasi wa magari yake ya kukokotwa, na askari wapandafarasi 12,000.