25 Siku zote za utawala wake Solomoni, watu wa Yuda na watu wa Israeli, toka Dani mpaka Beer-sheba, walikaa salama, kila mtu kwenye miti yake ya mizabibu na mitini.
26 Solomoni alikuwa na vibanda 40,000 kwa ajili ya farasi wa magari yake ya kukokotwa, na askari wapandafarasi 12,000.
27 Wale maofisa wake kumi na wawili, kila mmoja kwa mwezi aliopangiwa, walipeleka chakula cha kutosha kwa ajili ya mfalme na wale wote waliokula nyumbani mwake. Mahitaji yao yote yalitoshelezwa.
28 Zamu ya kila mmoja ilipofika, alipeleka pia shayiri na majani ya kulisha farasi na wanyama waendao kasi.
29 Mungu alimpa Solomoni hekima zaidi na akili kwa wingi; maarifa yake yalikuwa kama mchanga wa pwani, hayakuwa na kipimo.
30 Hekima ya Solomoni iliipita hekima ya watu wa mashariki na iliishinda hekima ya watu wa Misri.
31 Aliwashinda watu wote kwa hekima; aliwashinda Ethani, yule Mwezrahi, Hemani na Kalkoli na Darda, wana wa Maholi; na sifa zake zilienea katika mataifa yote jirani.