27 Wale maofisa wake kumi na wawili, kila mmoja kwa mwezi aliopangiwa, walipeleka chakula cha kutosha kwa ajili ya mfalme na wale wote waliokula nyumbani mwake. Mahitaji yao yote yalitoshelezwa.
28 Zamu ya kila mmoja ilipofika, alipeleka pia shayiri na majani ya kulisha farasi na wanyama waendao kasi.
29 Mungu alimpa Solomoni hekima zaidi na akili kwa wingi; maarifa yake yalikuwa kama mchanga wa pwani, hayakuwa na kipimo.
30 Hekima ya Solomoni iliipita hekima ya watu wa mashariki na iliishinda hekima ya watu wa Misri.
31 Aliwashinda watu wote kwa hekima; aliwashinda Ethani, yule Mwezrahi, Hemani na Kalkoli na Darda, wana wa Maholi; na sifa zake zilienea katika mataifa yote jirani.
32 Alitunga methali 3,000 na nyimbo 1,500.
33 Alizungumza habari za miti, kuanzia mwerezi ulioko Lebanoni, hata husopo, mmea uotao ukutani. Alizungumza pia juu ya wanyama, ndege, jamii ya wanyama wenye damu baridi watagao mayai, na juu ya samaki.